HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumapili, 5 julai 2009
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Wasiliana na Mwandishi
+447984584292
ansbertn@yahoo.comTuma barua-pepe
www.ngurumo.blogspot.comTembelea blogu
Mahakama ya Kadhi: Ahadi nzito iliyoshindikana

Ansbert Ngurumo

 

IWAPO hoja ya Mahakama ya Kadhi itafika mahali pa kuwakosanisha na kuwagombanisha Watanzania, mgogoro huo utakuwa umesababishwa na woga wa watawala wetu.

Mgogoro huo sasa unaanza kuchukua sura ya kidini, hasa baada ya Waislamu kuituhumu Serikali ya Awamu ya Nne kwamba inawasikiliza Wakristo katika masuala ya Waislamu.

Ni vema niseme tu mapema kwamba Waislamu wana hoja dhidi ya serikali na CCM lakini si dhidi ya Wakristo au Watanzania wa imani nyinginezo.

Sababu kuu ni moja. Serikali na CCM si taasisi za Wakristo. Na tamko la Waziri wa Sheria na Katiba kuhusu Mahakama ya Kadhi, si lake binafsi, ni la serikali, ambayo inagombana na chama chake kilichowaahidi Waislamu kupewa mahakama hiyo.

Lakini yapo mazingira mabaya yaliyojengwa na watawala ambayo Waislamu wanayatumia kujenga hoja yao. Watawala waliingiza siasa zao katika suala la kidini. Na Waislamu, kwa kutaka ulinzi wa kisheria wenye nguvu ya dola, wakakubali hoja ya watawala, na wakasubiri utekelezaji.

Watawala hawakuwa na nia ya kuitekeleza, bali waliitumia kama hoja ya ziada ya kuombea kura. Kwa hiyo, Waislamu wana haki ya kukasirika kwa kuwa wamegundua kuwa imani yao imetumiwa kwa maslahi ya kisiasa.

Kwa hiyo, Waislamu watapata ushindi mnono iwapo wataelekeza nguvu zao zote kwa watawala waliotoa ahadi. Watakuwa wanafanya makosa makubwa ya kimkakati iwapo watawaacha watawala na kuwashutumu wananchi wengine ambao ama wanashabikia au wanakejeli hoja hiyo.

Na hata kama kuna mazingira ya mzozo wa kimadhehebu, hayakuletwa na wafuasi au viongozi wa madhehebu hayo. Wanasiasa ndio wameyatumia makundi ya dini nchini kujipatia madaraka.

Kwa upande fulani, nitamtetea Rais Jakaya Kikwete, ambaye alitumia mbinu na mikakati mbalimbali ‘kuwashinda’ maaskofu, makasisi na wachungaji kabla na baada ya kuteuliwa kuwa mgombea urais.

Baadhi yetu tunajua nguvu kubwa aliyowekeza katika kuhakikisha anakubalika kwa viongozi wa dini za Kikristo. Hakuwa na shaka na kura za Waislamu wenzake. Na kama mwanasiasa yeyote, alikuwa na haki ya kuhakikisha anaitumia nguvu ya taasisi za Kikristo kupata anachotaka.

Kwa upande mwingine, mbinu ilikuwa inamjenga kuonekana kama daraja kati ya makundi makubwa haya mawili katika jamii. Na kwa jinsi baadhi yetu tunavyomfahamu, Rais Kikwete si mdini; bali mtu mwenye ustaarabu wa viwango vyake vinavyokubalika.

Kinachogomba, na kinachowaudhi Waislamu ni jinsi ambavyo anashindwa kukaa nao kujadili hatima ya suala hili, lakini yuko tayari kukaa na viongozi wa madhehebu mengine na kulitolea tamko. Hata kama ni kwa nia njema, mkakati wake si mzuri.

Kumbukumbu zangu zinanionyesha kwamba mara ya mwisho Rais alitoa kauli juu ya suala hili Novemba 17, 2007, siku ambapo niliandika katika safu hii na kuwataka Waislamu wambane yeye waachane na Mchungaji Christopher Mtikila.

Niliwaeleza Watanzania kwamba ahadi hii ya CCM ilikuwa ujanja wa kuombea kura. Nikawataka watafakari kuhusu nia, malengo na mkakati wa CCM, iliyomtumia mgombea urais Muislamu kuwaghilibu Waislamu; kwamba tumbane aliyetoa ahadi; na tumlazimishe aitekeleze.

Lakini nilionya, wakati huo, kwamba serikali hii, chini ya Rais Jakaya Kikwete, haikuwa na nia ya kuwapa Waislamu ofisi hiyo; na kwamba serikali ingefanya lolote linalowezekana ama kuiahirisha au kutoa ahadi nyingine mpya, tofauti na ya awali.

Kwa kusisitiza, niliandika hivi:

‘Ni wazi pia kuwa kama serikali ingeamua hata kesho kuwapa Waislamu mahakama yao isingeshindwa kufanya hivyo. Na kama inaona utaratibu wa kisheria kupitia bungeni unaleta mgogoro isingeshindwa kutamka kwamba Waislamu waanzishe mahakama yao wenyewe bila kuishirikisha serikali.

Lakini inajua kwa nini inanyamaza. Haitoi uamuzi kwa sababu haina nia tena ya kuunda mahakama hiyo. Na imepata bahati sasa ya kuwagawa Waislamu…

Itawachukua Waislamu muda mrefu kugundua kuwa wanapambana na mtu asiyehusika na ucheleweshaji wa ahadi ya Rais Kikwete na CCM; na sababu ni moja. Wameamua kusikiliza hotuba nzuri. Hawajapata ujasiri wa kudai matendo ya dhati.

Najua fika kwamba Rais Kikwete binafsi hakupenda wala hapendi suala hili la Mahakama ya Kadhi katika ilani ya uchaguzi ya CCM.

Bahati mbaya hakushiriki kuiandaa, lakini alishiriki kuinadi. Naamini hata yeye leo hajui ni nani aliliingiza suala hilo kwenye ilani. Na hata wakimpata leo, hawataondoa ukweli kwamba yeye (Kikwete) ndiye aliyezunguka nchi nzima analipigia debe.

Ndiye anayepaswa kudaiwa maelezo. Hawezi kubadili ilani ya CCM leo. Waislamu hawawezi kukubali kutumiwa kwa ajili ya kura na baadaye kupuuzwa tu kwa sababu ya hisia binafsi za viongozi wale wale.

Wanachopaswa kufanya ni kumbana Kikwete. Na kama watasubiri hotuba nzuri kuhusu hili, wampe nafasi ataibuka siku moja na maneno matamu ya kuahirisha azma yao. Sijui kama watapiga makofi kumshangilia au watapaza sauti kumzomea.’

Wengi walinielewa, wakati huo; wachache waliitazama hoja yangu kwa macho ya kidini. Lakini baada ya tamko la sasa la serikali, lililotolewa na Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, kwamba serikali haitaunda Mahakama ya Kadhi na badala yake itatafsiri sheria za Kiislam na kuzijumuisha kwenye sheria za nchi, ili zitumike kwenye mahakama za kawaida hapa nchini, naamini sasa tunaanza kuelewana.

Wanaomlaumu waziri kama mtu binafsi wanakosea. Waziri ni mjumbe tu; na mjumbe hauawi! Na wanaoilaumu imani ya waziri wanatenda kosa jingine. Yeye ametumwa na serikali inayoongozwa na chama chake. Huo ndiyo msimamo wao.

Kwa hiyo, watu wanaopaswa kung’ang’aniwa ni watawala. Kwanza, hoja hii ni ya kidini, lakini watawala wameigeuza hoja ya kisiasa. Na wakati mwingine walipoamua kuijadili kidini walitumia uwanja usio mwafaka, kama alivyofanya Rais Kikwete Novemba 17, 2007 mbele ya maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT).

Siku hiyohiyo niliposema Waislamu wambane yeye, rais mwenyewe alijitokeza, akawaambia maaskofu wa KKKT kuwa yeye hahusiki na suala la Mahakama ya Kadhi; akawataja watu waliolitetea na kuliingiza katika mjadala wa chama chake.

Baadhi yetu tulimkosoa kwamba kwa kauli hiyo alifanya makosa mawili. Kwanza, alipaswa kuzungumza hivyo mbele ya Waislam ili wamhoji ajibu maswali yao. Kilichompleka kwa maaskofu kujadili hoja ya Waislamu ndicho kinawapa nguvu baadhi yao kumuona Rais anatumiwa na Wakristo au anawaogopa huku akiwapuuza wahusika katika suala hili.

Pili, licha ya ukweli kwamba yeye hakuhusika kuliingiza suala hili kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ndiye aliyeinadi kwa umma na kutoa ahadi ambayo Waislamu bado wanataka itekelezwe.

Kwa hiyo, kama Waislamu wanalalamikia kutumiwa, aliyewatumia ni yule aliyewapa ahadi wakampa kura. Kama hakushiriki kuandika ilani si utetezi tosha wa kumtoa kwenye lawama, labda kama anataka kufuta ilani nzima, maana ndiyo hiyo anayodai anaitekeleza yeye – na si yeye aliyeiandika (na hatukumtarajia aiandike).

Zaidi ya hayo, ndiye mwenyekiti wa CCM na rais wa nchi. Kama amegundua makosa ya ilani yake katika suala hili, ni kipi kinamzuia kukutana na Waislamu akawaeleza msimamo wake mpya (kwamba aliinadi hoja hiyo kimakosa), akasikia hoja zao moja kwa moja, akajibu maswali yao na kuwaondolea wasiwasi?

Kwa nini woga wa rais kukutana na Waislamu usababishe chokochoko za kijamii kati ya Waislamu na waamini wa madhehebu mengine? Kwa nini madaraka yao ya kisiasa yawe sababu ya kuivuruga jamii kwa misingi ya tofauti ya kidini?

Rais na wapambe wake lazima wajue kwamba suala hili litawatafuna hata kama wanadai si wao walioliingiza kwenye ilani, lakini kipimo tunachotumia kupima utekelezaji wake wa ahadi nyingine ndani ya ilani ya chama chake, ndicho hicho tunachotumia kupima kushindwa kwake kutekeleza ahadi hii ya ofisi ya Kadhi Mkuu.

Si kwamba hatujui ugumu au utata wa kisheria, kikatiba na kijamii unaoweza kujitokeza; wala si kwamba sisi ni mashabiki wa suala hili; bali tunataka watawala wawe waungwana, maana halikuingizwa ghafla kwenye ilani.

Na haiwezekani kwamba wasioitaka (akiwamo rais) hawakuliona muda wote huo hadi walipoingia madarakani. Walijua wanachofanya; na hapa walitaka kuwatumia Waislamu kuzoa kura za ushindi wa kishindo. Sasa kama ni waungwana, walipaswa kutimiza ahadi yao, maana Waislamu walishatimiza wajibu wao wa kupiga kura.

Ipo methali ya Kiarabu isemayo: ‘Ahadi ni mawingu, utekelezaji wake ndiyo mvua.’ Tunataka rais akubali mvua inyeshe, hata kama itamlowesha, maana yeye ndiye alitengeneza mawingu hayo.

Kwa kuahirisha hoja yao na kutoa tamko jipya sasa, Kikwete anatafuta fursa ya kutekeleza ujanjaujanja wa Mwanafalsafa machachari wa Kitaliano wa karne ya 16, Niccolo Machiavelli, kwamba ‘mfalme hakosi sababu za msingi za kutotimiza na kuvunja ahadi yake.’

Hii ndiyo maana ya kauli ya serikali bungeni, kupitia kwa Waziri Mathias Chikawe wakati akiwasilisha makadirio na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2009/10, wiki hii, kwamba:

''Hivi sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanzisha mchakato wa kukusanya mawazo na maoni kutoka kwa viongozi wa madhehebu yote ya Dini ya Kiislamu kwa nia ya kuorodhesha misingi ya Dini ya Kiislam, hususan ile inayohusu sheria binafsi kwa madhumuni ya kuihuisha misingi hiyo katika sheria za nchi, kwa kuzingatia sheria ya The Islamic Law Act, sura ya 375 ya mwaka 1964.''

Hiki ndicho wanachokipinga Waislamu, na ndicho kinawalazimisha kuonyesha hasira zao kwamba hawataipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, hasa kama atakayegombea ni Rais Kikwete.

Wanasema hivyo wakijua kuwa ndiye atakayegombea; maana maandalizi yameshaanza. Wasichojua ni kwamba yeye alijua hisia zao mapema, na serikali imeamua kuzikabili mapema mwaka huu kuliko kusubiri mwakani ili kupoza hasira zao pole pole kuelekea uchaguzi mkuu.

Sina hakika kama serikali haijaweka mkakati mbadala wa kuwalegeza na kuwagawa ili ichote kura zao kwa staili nyingine, na ahadi nyingine.

Imewachukua muda mrefu Waislam kugundua ujanja wa wanasiasa. Kauli ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) iliyotolewa na Mufti Sheikh Mkuu, Issa bin Shaaban Simba kwamba ‘Rais Kikwete alikuwa akitulaghai ili tumpigie kura’ ilipaswa kutolewa siku nyingi. Labda ingekuwa imewasaidia kumsukuma na kumlazimisha kuzungumza nao ana kwa ana.

Sasa wakati umefika, rais aache woga, akutane na Waislamu awasikilize kwa makini; maana sasa ni zamu yako kusikilizwa.

Awaombe radhi kwa kuwatumia katika kampeni kwa suala linalohusu imani yao, ambalo kama wangeambiwa mapema wasingeshindwa kujianzishia Mahakama ya Kadhi Mkuu kama yanavyofanya madhehebu mengine ya dini.

Ajue kwamba kwa jinsi upepo unavyokwenda sasa, wapo Waislamu ambao wanalijadili suala hili bila kutazama udhaifu wa watoa ahadi; bali nguvu ya madhehebu mengine, hasa ya Kikristo, ambayo wanadhani ndiyo yamesababisha serikali kuwakatalia jambo lao.

Na wapo wananchi wa madhehebu mengine wanaoshangilia kushindwa kwa ahadi hii kwa sababu za kidini au za kisiasa, kwamba imesaidia kuonyesha udhaifu na uongo wa serikali inayoongozwa na CCM; na jinsi inavyotii vitisho vya waliokataa Mahakama ya Kadhi.

Naona, nasikia na kuhisi hasira za Waislamu. Ni kweli wameonewa; si tu kwa kunyimwa walichoahidiwa, bali kwa kutumiwa kama ngazi ya wanasiasa kupata madaraka.

Kinachobaki sasa, ni jamii kutazama hatima ya mvutano wa Waislamu na CCM. Utakuwa mvutano wa mabavu au wa hoja? Zitakuwa hoja za kisiasa au za za kidini? CCM itafanikiwa kuwagawa katika makundi na kushinda tena?

Je, wako tayari kushindwa kila harakati zao dhidi ya wanasiasa watawala? Je, CCM ipo tayari kukiri kosa na kuwaomba radhi Waislamu, na kuahidi kutotumia tena masuala nyeti ya imani yao katika majukwaa ya kisiasa?

Je, Waislamu (katika hasira walizo nazo sasa) wanaelewa kuwa ‘wabaya’ wao katika hili si Wakristo bali wanasiasa wajanjawajanja wanaofikiri kwamba njia yoyote inayoweza kuwafikisha madarakani ni halali wakati wa kampeni?

Je, serikali inajua kuwa iwapo msimamo wake utaleta mgawanyiko na uadui wa kidini katika jamii, serikali ndiyo itawajibika kwa kuchochea migogoro ambayo ingeweza kuahirishwa kwa uungwana wa watawala?

Matokeo mabaya yanaweza yasitokee katika utawala wake, lakini Rais Kikwete akiondoka madarakani bila kuliweka sawa suala hili atakuwa anajivunia kuacha urithi gani wa chokochoko za kidini?

Je, Rais Kikwete bado anatafuta wachawi (walioliingiza suala hili kwenye ilani) wa kubebesha lawama au sasa ameshakomaa na kujua kwamba yeye ndiye rais wa nchi, mwenyekiti wa CCM, na ndiye anapaswa kuwajibika kwa masuala nyetu kama haya?

Je, wale wanaoipongeza CCM kwa kutekeleza ilani yake kwa silimia 100, wanajumuisha na udhaifu huu wa Mahakama ya Kadhi? Au hii nayo ni ahadi iliyotekelezwa? Iwe iwavyo; Watanzania wanataka majibu yaliyokamilika.



juu