BONDIA Paschal Ndomba ‘Kimondo’ wa Kyela, Mbeya juzi alimkalisha Yusuf Jibaba wa Dar es Salaam kwa KO raundi ya nne katika pambano lisilo la ubingwa lililopangwa kuwa la raundi nane.
Pambano hilo la uzani wa kati, lilifanyika kwenye ukumbi wa Chunga ulioko Kasumuku, mpakani mwa Tanzania na Zambia na lilitanguliwa na mapambano kadhaa.
Hamad Mwakanyemba ‘bad boy’ wa Kyela alimshinda kwa pointi Seif Said wa Tukuyu, Shaban Mohammed akatoka sare na mwenzake Watson Nyasa wote kutoka Kyela.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Kasumulu jana, Kimondo, alisema kuwa mgeni rasmi katika pambano hilo Geofrey Ukungu, ameahidi kushirikiana na Humprey Mango, kumuandalia pambano kati yake na bingwa wa dunia wa uzani huo mwenye mataji ya UBO na ICB, Francis Cheka wa Morogoro.
“Bwana nashukuru mgeni rasmi katika pambano hili Geofrey Ukungu, amesema yuko tayari kushirikiana na mratibu kuandaa pambano langu na Cheka,” alisema Kimondo.