MFUNGAJI bora wa Ligi Kuu ya Bara msimu uliopita, Mussa Hassan Mgosi, leo anatarajia kwenda Zanzibar kuungana na wenzake waliotanguliwa tangu juzi kwa kambi ya kujiandaa na mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Yanga Agosti 14 na Ligi Kuu itakayoanza Agosti 21.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo, Mgosi hakuweza kuripoti kwa wakati katika kikosi hicho kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja, lakini kwa sasa amepona hivyo kuwafuata wenzake Zanzibar.
Kuhusu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mzambia Patrick Phiri, anatarajiwa kuwasili siku yoyote kuanzia leo baada ya kupewa siku moja ya kufanya hivyo na uongozi.
Aidha, Ndimbo alisema kocha wa viungo wa Simba, Sylersaid Mziray, naye anatarajia kuelekea Zanzibar leo kwa ajili ya kuwanoa vijana hao.
Juzi, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, alikaririwa akisema uvumilivu wao dhidi ya Phiri unaelekea ukingoni, hivyo akizidi kuwa kimya wataangalia uwezekano wa kuvunja mkataba na kocha huyo.