HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumanne, 27 julai 2010
Yaliyopita
Pekua Tovuti
TAKUKURU maneno yametosha, tunataka vitendo sasa

 

TUMEPOKEA kwa mshtuko habari za kukamatwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, Betty Machangu, kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya utoaji rushwa.

Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT- CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Miriam Kaaya, naye ni miongoni mwa wanaotuhumiwa kumsaidia Machangu kugawa fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT unaotarajiwa kufanyika kesho mkoani Kilimanjaro.

Wengine waliokumbwa na mkasa huo ni Katibu wa UWT Manispaa ya Moshi, Hadija Ramadhan na Hawa Sultan, ambaye inadaiwa ni mjasiriamali.

Taarifa hizo zimetushtua, kwa kuwa viongozi wana jukumu kubwa la kulinda na kuzitekeleza sheria mbalimbali zilizopo hapa nchini ili wananchi nao waige mfano wa viongozi hao.

Tunaamini kuwa viongozi ni kioo cha jamii, hivyo wanapaswa kufanya matendo yao huku wakitambua watu wanaowaongoza wapo nyuma yao wakiwafuatilia kwa kila wanachokifanya.

Tunapenda kuchukua fursa hii kuipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa kumkamata kiongozi huyo, lakini tungependa kuona vitendo zaidi kuliko maneno yanayoishia kwenye vyombo vya habari.

Haitakuwa na maana kama TAKUKURU wataendelea kuwaumbua viongozi wala rushwa bila ya kuwafikisha mahakamani, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wakiendelea kupalilia rushwa.

Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kuwa taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa kuwaogopa watu au kuwapendelea, huku ikiwakandamiza wengine, hivyo ni vema ikauthibitishia umma kuwa inafanya kazi zake kulingana na matakwa ya sheria.

Tunaamini kuwa kama TAKUKURU na wananchi wakishirikiana kwa pamoja tunaweza kupunguza na kutokomeza tatizo la utoaji na upokeaji rushwa, hasa nyakati za uchaguzi.

Matumizi ya fedha limekuja jambo la kawaida hivi sasa, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limeathiri upatikanaji wa viongozi safi wenye kuwahudumia wananchi na badala yake kuwekuwapo na viongozi wanaopatikana kwa kununua kura.

TAKUKURU wamekuwa wakitoa taarifa kuwa kuna vigogo kadhaa wanawahoji kwa sababu ya kutoa zawadi ambazo zina mazingira ya rushwa, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Tunaamini kuwa moto huu waliouanzisha TAKUKURU hautaishia kwa mkuu huyo wa wilaya, bali utafika mpaka kwa mawaziri, wabunge na viongozi wote wanaoendekeza vitendo vya rushwa.

Tusingependa taasisi hiyo ionekane kali kwa viongozi wadogo huku ikiwaachia wale wakubwa, ambao wamekuwa na mbinu mbalimbali za kutoa rushwa ili wachaguliwe kwenye nafasi wanazoziwania.

Mwisho, tunawaomba wananchi washirikiane na taasisi hiyo ili kukomesha matukio ya rushwa, ambayo hivi sasa imeota mizizi na kuathiri maendeleo ya nchi.



juu