HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumanne, 27 julai 2010
Yaliyopita
Pekua Tovuti

SMZ yakemea wanaonunua, kuuza kura


na Hassan Shaaban, Zanzibar

 

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imewaonya baadhi ya wananchi wanaogeuza uchaguzi kuwa msimu wa mavuno kwa kujihusisha na vitendo vya kupokea rushwa kutoka kwa wagombea, kinyume cha sheria.

 Onyo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Katiba na Utawala Bora, Ramadhan Abdalla Shaaban, alipokuwa akifungua mafunzo kwa Polisi, makatibu tawala na waandishi wa habari yaliyohusu sheria ya gharama za Uchaguzi, yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

 Waziri Shaaban alisema kutokana na Serikali ya Muungano kuelewa tatizo hilo ndiyo maana ikaamua kuanzisha sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010, ili wananchi wapate nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka bila ya ushawishi wa rushwa.

 Alisema kabla ya kuja kwa sheria hiyo wenye fedha ndio waliokuwa na nafasi kubwa ya kuchaguliwa na kushika nafasi za uongozi, kitendo ambacho ni kinyume na misingi ya demokrasia na utawala bora.

 Akiwasilisha mada kuhusu sheria ya gharama za uchaguzi, Mratibu wa Elimu kwa Umma, Zakia Stephano, alisema sheria hiyo ni ukombozi kwa wananchi kwa vile tayari imeshaanza kuzaa matunda tangu mchakato wa wagombea kuanza kufanyika. 

Alisema kwamba Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na rushwa kimeanza kupta mafanikio makubwa katika kudhibiti rushwa kwenye uchaguzi na kutoa mfano wa hivi karibuni kuwa kuna watu wamekimbia majungu ya awali baada ya kusikia askari wa TAKUKURU wamefika.

Hata hivyo, alisema wananchi wanapaswa kuisoma vizuri na kuielewa sheria hiyo, kwa sababu mtoa rushwa na mpokeaji kwa mujibu wa sheria wote ni wakosaji.

 Alisema wagombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano na ubunge wamebanwa na sheria hiyo kwa vile imeweka kiwango maalumu cha idadi ya watu wanaopaswa kuambatana na mgombea wa nafasi hizo katika timu yake.



juu