HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumanne, 27 julai 2010
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Ajali yaua 10 Tanga


na Bertha Mwambela, Korogwe

 

WATU kumi wamekufa na wengine watatu wamejeruhiwa baada ya magari mawili waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na kuwaka moto.

Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa moja na nusu usiku katika barabara ya segera eneo la Hale, ikilihusisha gari aina ya lori Scania na basi dogo (Hiace).

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Liberatus Sabas, alisema lori hilo lenye namba T. 514 ART na tela T 503 ASH lilikuwa likiendeshwa na Thadei Njau (42), mkazi wa Moshi na Hiace yenye namba za usajili T. 569 ilikuwa ikiendeshwa na Faridi Mndeme (30) mkazi wa Makorora, Tanga.

Kamnda Sabas alisema ajali hiyo ilitokea wakati dereva wa lori alipokuwa anataka kuipita pikipiki yenye namba T 489 AYM katika kona kali huku akiwa kwenye mwendo mkali, ndipo alipogongana uso kwa uso na Hiace hiyo.

Alisema katika ajali hiyo madereva wa magari yote mawili walikufa papo hapo na abiria wengine wanane pia walifariki dunia.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Mistri Ally (23) mkazi wa Segera, Juma Bakari (28) mkazi wa Michungwani na Msafiri Msenga, huku maiti nyingine tano bado hazijatambuliwa na zimehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo.

Waliojeruhiwa ni George Samweli (25), Ibrahim Ally (36) na Helena Juma, wote wakazi wa Michungwani na wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Muheza.

Kamanda Sabas ametoa wito kwa madereva wote mkoani hapa kuendesha magari kwa kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani ili kuepuka ajali za mara kwa mara.

“Ajali nyingine zinaweza kuepukika iwapo madereva wetu watakuwa makini na kuzifuata sheria za usalama barabarani,” alisema.



juu