WIMBI la askari polisi kuendelea kujiua limeendelea kutikisha ndani ya jeshi hilo, baada ya askari polisi mwingine mwenye namba G 13, PC Mashauri (24), kujipiga risasi mbili.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Evarist Mangalla, alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Hili ni tukio baya la tatu kutokea kwa kipindi cha wiki moja baada ya askari aliyekuwa mkufunzi katika Chuo cha Polisi Dar es Salaam, Konstebo Noel Njega, kujipiga risasi akiwa kazini.
Baada ya tukio hilo, askari mwingine WP Susana naye alijipiga risasi akiwa chini ya ulinzi wilayani Tarime mkoani Mara, baada ya kile kilichoelezwa kuwa aliupoteza msafara wa Rais Jakaya Kikwete.
Kamanda Mangalla alisema PC Mashauri alijipiga risasi akiwa Ikulu ndogo ambako ni nyumbani kwa Mkuu wa Mkoa Iringa, kutokana na wivu wa mapenzi.
PC Mashauri alikuwa na mpenzi wake wa zamani ambaye walikuwa wameachana muda; siku ya tukio akiwa kazini alimuona mwanamke huyo na mwanaume mwingine ambaye ni mfanyakazi wa taasisi ya Bay Port Dar es Salaam na hasira zikampanda.
“Tukio hili lilitokea juzi usiku majira ya saa 3 usiku, baada ya PC Mashauri kujipiga risasi mbili chini ya kidevu, eneo la Ngangilonga, huku akiliacha lindo lake la benki ya CRDB likiwa tupu,” alisema Kamanda Mangalla.
Kwa mujibu wa RPC Mangalla, inadaiwa marehemu huyo alijiua kwa sababu ya wivu wa kimapenzi kwa mpenzi wake ambaye naye ni askari WP 7137 Zuhura.
“Askari huyo kabla ya kujiua alikuwa amepangiwa lindo katika Benki ya CRDB, lakini aliliacha lindo lake na kwenda nyumbani kwa mpenzi wake huyo wa zamani ambaye anaishi Kihesa mtaa wa Mafifi; alipofika huko, alimkuta mwanaume aliyetambulika kwa jina la Sunday Tumaini na kuanza kuwatishia kuwapiga risasi wote wawili kabla ya mwanamke huyu kufanikiwa kumpokonya silaha hiyo,” alisema Kamanda Mangalla.