SERIKALI imesema Mahakama ya Kadhi itaanza katika mwaka wa fedha 2010/11 baada ya jopo la wanazuoni wa Kiislamu wanaoziangalia na kuzihuisha sheria za Kiislamu kukamilisha kazi hiyo.
Jambo hilo lilibainishwa jana bungeni na Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe wakati akisoma hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2010/2011 ambapo ameliomba Bunge limuidhinishie kiasi cha sh bilioni 116.8
Alisema kuwa jopo hilo linaziangalia na kuzihuisha sheria za Kiislamu zinazohusiana na ndoa, mirathi na urithi kwa madhumini ya kuziorodhesha ili zitambuliwe chini ya sheria za dini ya Kiislamu (Islamic Law resstatment act).
Aliongeza kuwa jopo hilo lilianza kazi hiyo baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kukutana na Mufti, Sheikh Mkuu, Issa Bin Shaaban Simba, na kukubaliana kuwa waanzishe mchakato wa Mahakama ya Kadhi.
Wakati serikali ikitoa tamko hilo kambi ya upinzani bungeni, imesema Waislamu wanapata shida kwa kukosa mahakama hiyo ambapo hawawezi kuamua mambo yao ikiwemo mirathi, ndoa na talaka.
Akisoma makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya Sheria na Katiba, msemaji wa kambi ya upinzani kwa wizara hiyo Fatma Maghimbi alisema ndoa ya Kiislamu hufungishwa na shekhe lakini kuvunjwa kwa ndoa hiyo kunapaswa kufanywa na Mahakama ya Kadhi.
“Kwa mantiki hiyo serikali inawatia Waislamu katika dhambi pale inapowasababishia kuvunja ndoa zao katika mahakama ambazo si za kadhi,” alisema Maghimbi.
Alisema, inawezekana serikali ya CCM inadhani kuwa Waislamu ni wachache hapa nchini, ukweli ni wengi lakini hata kama ni wachache ni lazima dhana ya demokrasia itekelezwe.