SIKU tatu baada ya wananchi wa Kata ya Mbarika, wilayani Misungwi, mkoani Mwanza kuvamia kituo cha polisi na kuua majambazi watatu, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema ameanza kulikarabati upya jeshi hilo.
Tanzania Daima imethibitishiwa hilo; ukarabati wa jeshi hilo umelenga kuvipunguza kwa kuvifutilia mbali baadhi ya vituo vidogo visivyokuwa na silaha wala askari wa kutosha.
Wakati IGP Mwema akipanga kuvifumua vituo hivyo, jeshi la polisi mkoani Mwanza halijamkamata mtu hata mmoja kuhusiana na tukio la kuvamia na kuvunja kituo cha polisi Mbalika na kuua watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.
Akithibitisha yote hayo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanmza, Simon Sirro (RPC), alisema IGP Mwema yupo katika mikakati ya kupunguza utitiri wa vituo vidogo vidogo vya polisi, kwani vimeonekana havina faida kwa wananchi.
“Unajua vituo hivi vidogo visivyokuwa na silaha havina faida kwa maana hiyo mkuu wa polisi kwa sasa yuko katika mpango wa kuvipunguza.
“Mkakati huu madhumuni yake ni kuwa na kituo kimoja kila kata chenye silaha na askari wa kutosha,” alisema Kamanda Sirro.
Mei 27 mwaka huu majira ya saa 1:30 jioni, wananchi wa Mbalika, wilayani Misungwi mkoani hapa, walivamia na kuvunja kituo cha Mbalika kisha kuua watuhumiwa.
Moja ya sababu za wananchi hao kuvamia na kufanya mauaji katika kituo hicho, inaonekana ni kutokuwa na silaha pamoja na askari wa kutosha kituoni hapo na kumshtua IGP Mwema.
Kamanda Sirro, alipoulizwa mikakati ya kupunguza vituo hivyo, alisema hana jibu anayepaswa kulizungumzia ni IGP Mwema pekee.
Tanzania Daima, ilipomtafuta IGP Mwema kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi, simu yake ilipokelewa na msaidizi ambaye alidai yuko mkutanoni.
“Afande IGP yupo kikaoni huku Kilolo mkoani Iringa; atakuwa Dar es Salaam kesho (leo),” alisema msaidizi huyo.
Wakati huohuo, habari kutoka Kahama, mkoani Shinyanga, zinasema watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wametaka kijiji kwa muda wa saa mbili na kupora mamilioni ya fedha nyumba moja baada ya nyingine.
Akizungumza na Tanzania Daima, Diwani wa Kata ya Kilago, Lucas Makulumo, alisema watu hao wanaosadikiwa kuwa majambazi wanaokisiwa kuwa sita, huku wakiwa na silaha zikiwemo nondo, mapanga na bunduki, walivamia kijiji cha Iyenze mwishoni mwa wiki, majira ya saa 5 za usiku na kujeruhi watu saba.
Alisema majambazi hayo yaliteka kijiji hicho kwa staili ya aina yake ya kuvamia huku wakipiga yowe zilizodumu kwa saa mbili.
Alisema katika vurumai hizo, majambazi hayo yalifanikiwa kuteka kiasi cha sh milioni tano, vocha za simu zenye thamani ya sh 200,000, simu kadhaa za mkononi na baiskeli moja.
“Kinachonisikitisha zaidi ni polisi kuchelewa kufika eneo la tukio, hali iliyowapa fursa wahalifu kufanya watakalo,” alisema Makulumo.
Mmoja wa wanakijiji walioibiwa kisha kujeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Madafu Maganga (40), alisema majambazi hayo yalifaulu kukiteka kijiji hicho kwa urahisi baada ya kuwapa tishio wanakijiji kwa kupiga hewani risasi mfululizo kitendo ambacho kiliwafanya wapate hofu na kushindwa kujipanga kukabiliana nao.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Heleni Yesaya, alikiri kupokea wagonjwa saba kutoka kijiji cha Iyenze, wakiwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.
Alisema kati ya majeruhi hao, nane wamelazwa katika wodi namba nane huku watatu wakiruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu. Waliolazwa ni pamoja na Madafu Maganga (40), Simon Ndaki (45), Emmanuel Nzali (30) na Dotto Migilimo (34).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Daud Siasi, alithibitisha kutokea tukio hilo na kwamba juhudi za kuwasaka majambazi zinafanyika kwa kasi ya aina yake.
Wiki moja iliyopita, Kamanda Tossi akiwa na kikosi chake aliendesha operesheni ya wiki mbili na kufaulu kukamata watu zaidi ya 50 wakiwemo waliomteka mbunge wa Bukombe.