HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
alhamis, 5 novemba 2009
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Sheria mpya za kazi Tanzania

Mwandishi Wetu

 

KAZI ni msingi wa maendeleo ya mtu yeyote mwenye uwezo wa kimwili na kiakili kutegemea na mahitaji ya kazi yake.

Kazi ndio msingi madhubuti wa uchumi wa kibepari unaotawala dunia yetu kwa sasa.

Hata hivyo kazi inayotokana na makubaliano kati ya pande mbili, yaani mfanyakazi na mfanyiwa kazi, haina budi kulindwa na sheria.

Nchi nyingi ulimwenguni kwa kutambua umuhimu wa kazi katika maendeleo ya nchi zao na wananchi wao, wameona umuhimu wa kuzifanyia mabadiliko sheria zao za kazi ili zikidhi matakwa yasasa ya jamii kwa ujumla.

Mnamo mwaka 2004, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilitunga na kupitisha sheria mpya za kazi ili kukidhi mahitaji ya mfumo wa kiuchumi na kijamii tulionao katika dunia ya leo.

Kwa sasa, hizi ndizo sheria kiongozi za kazi hapa Tanzania ambazo ni Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, namba 6 ya mwaka 2004; na Sheria ya Taasisi za Kazi, namba 7 ya mwaka 2004.

Ujio wa sheria hizi umefuta na kuondoa mlolongo wa sheria za kazi za zamani kama Sheria ya Kazi, Sheria ya Mahakama ya Kazi ya Tanzania na Sheria ya Ulinzi wa Ajira yaani ‘Security of Employment Act.’

Sheria hizi zinawahusu wafanyakazi wanaofanya kazi katika sekta binafsi na ile ya umma kwa Tanzania Bara pekee, isipokuwa hazitumiki kwa Jeshi la Polisi, Magereza, Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 2 kifungu kidogo cha kwanza cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.

Kwa ujumla, sheria hizi hazitambui na kwa hakika zinakataza ajira za watoto, kazi za shuruti, ubaguzi wa aina yoyote kazini na inaruhusu kuanzisha au kujiunga na vyama vya wafanyakazi na waajiri.

Hizi ni haki za msingi na vilevile ni sehemu ya ulinzi wa ajira. Malengo ya msingi ya sheria hizi kama yalivyoainishwa na sheria namba 6 ya mwaka 2004, ni kuweka utaratibu wa kuzuia na kutatua migogoro ya kikazi kwa njia ya kuunda vyombo vya kushughulikia masuala ya kazi na ajira pamoja na kuelekeza wajibu, madaraka na kazi kwa vyombo hivyo.

Vilevile kuainisha haki za msingi za wafanyakazi na pia kuweka viwango vya msingi kufuatana na mikataba ya kimataifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambayo imeridhiwa na Serikali ya Tanzania.

Kwa mujibu wa kifungu cha 5; kifungu kidogo cha 6 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, ni jukumu la serikali kupitia Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana kuhakikisha kuwa waajiri wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na matakwa ya mikataba ya kimataifa ya ILO.

Hivyo basi, kwa mujibu wa kifungu 7(2) mwajiri anatakiwa awe na sera na mpango wa utekelezaji wa fursa sawa kwa wote, aajiri kwa kamishna wa kazi, atoe fursa sawa na kuondoa ubaguzi katika sehemu za kazi na pia achukue hatua za makusudi katika kutoa ujira ulio sawa kwa wafanyakazi wa kike na wa kiume pale wanapofanya kazi ya aina moja.

Hata hiyo, sheria hii haitakuwa na ubaguzi kama mwajiri atatoa kipaumbele kwa wafanyakazi wa kike au wa kiume ili kukidhi mahitaji ya jinsia mojawapo au kuziba pengo lililoachwa wazi.

Sheria hii ya kazi, imeweka viwango vya ajira, saa za kazi, malipo ya ujira, kiinua mgongo, likizo, kuacha au kuachishwa kazi na aina mbalimbali za mikataba ya ajira.

Mikataba hii inaweza kukoma kwa kutolewa notisi au bila notisi. Ukomo wa ajira ulidadavuliwa vizuri katika maamuzi ya Mahakama Kuu ya Tanzania katika shauri la M/S Burke Coffee Estate Limited dhidi ya The Senior Labour Officer ( 1976- LRT 43) ni kwamba kitendo cha upande mmoja kati ya mwajiri au mwajiriwa, kuvunja mkataba wa kazi pasi na idhini ya upande mwingine.

Hivyo basi kwa mujibu wa sheria hizi, kuna aina za ukomo wa ajira, ule usio halali kisheria na ukomo halali kisheria.

Ukomo usio halali kisheria

Huu ni ukomo wa ajira ambao hautambuliki kisheri na si halali, huu ni ukomo wa ajira unaokwenda kinyume na taratibu na haki kama vile: kutokuwa na sababu za msingi za kukomeshwa ajira ya mfanyakazi, kutompa mfanyakazi haki ya kusikilizwa na fursa ya kuwakilishwa.

Hivyo kama kuna ukomo wa ajira ambao unaangukia katika maelezo hayo hapo juu, basi ni wazi kabisa huo utakuwa ukomo usio halali mbele ya sheria.



juu